Urusi - Wikipedia, Kamusi Elezo Huru

Demografia

Warusi asilia ni 81%, lakini kuna makabila mengine 160 katika shirikisho, ambayo yanatumia lugha 100 hivi[1] (angalia orodha ya lugha za Urusi).

Kufuatana na sensa ya mwaka 2002 kulikuwa na watu milioni 142.6 wasemaji wa Kirusi, wakifuatwa na wasemaji wa Kitatari milioni 5.3 na Kiukraina milioni 1.8.[2]

Lugha rasmi na ya kawaida ni Kirusi kwenye maeneo yote ya Shirikisho la Kirusi lakini katiba ya nchi inatoa kibali kwa Jamhuri za shirikisho kujiamulia lugha rasmi ya nyongeza kwa eneo lao pamoja na Kirusi.[3]. Kuna pia "maeneo huru" ya pekee yenye lugha zao pamoja na Kirusi.

Dini

Mchoro wa Ivan Eggink ukionyesha Vladimir Mkuu akisikiliza mapadri wa Kiorthodoksi, huku mjumbe wa Papa akinuna pembeni.
Ubatizo wa Vladimir, mchoro wa ukutani wa Viktor Vasnetsov

Warusi wengi kabisa walikuwa wafuasi wa Ukristo wa Kiorthodoksi hadi mapinduzi ya 1917/18. Katika mapokeo yao wenyewe ni Mtume Andrea aliyeleta mara ya kwanza imani hiyo hadi Urusi.[4].

Chanzo cha mapokeo hayo yalitokeo kwenye eneo la Ukraine ya leo ambako mnamo mwaka 988 mtemi wa Kiev Vladimir Mkuu alipokea ubatizo kutoka kwa mapadre wa Kanisa la Bizanti uliofuatwa na ubatizo wa familia na wananchi wa Kiev[5].

Kanisa la Kiorthodoksi liliendelea kuwa dini rasmi katika milki za Kirusi hadi mapinduzi ya 1917. Wakomunisti walioshika utawala mwaka ule walikataa dini zote [6] Urusi pamoja na Umoja wa Kisovyeti ilikuwa nchi ya kwanza iliyoamua kufuata uatheisti kama itikadi kuu[7] [8][9] Serikali ya kikomunisti ilinyang'anya mali na majengo ya Kanisa, magazeti yake yalishambulia mafundisho ya dini, uatheisti ukafundishwa shuleni na waumini wakahangaishwa.[10] Makanisa mengi yaligeuzwa kwa matumizi ya ghala, ukumbi wa michezo na kadhalika au kubomolewa.

Mapadre, maaskofu na maimamu mara nyingi walikamatwa, kutupwa gerezani au kutumwa kwenye makambi ya GULAG. Kati ya miaka 1922 hadi 1926 jumla ya maaskofu 28 na mapadre zaidi ya 1,200 waliuawa. Wengi sana zaidi walidhulumiwa.[11]

Dini za awali ziliendelea chini ya ukomunisti lakini kwa matatizo makubwa. Waumini waliweza kusali kwao nyumbani na katika makanisa na misikiti michache iliyobaki. Wakati wa Vita Kuu ya Pili mateso yalipungua kidogo kwa sababu Joseph Stalin alitaka kuwaunganisha wananchi wote chini ya uongozi wake katika juhudi za vita.

Baada ya ukomunisti kuanguka mnamo 1990 jumuiya za kidini zimepata uhai mpya. Wafuasi wa dini hawahesabiwi katika sensa, hivyo kuna makadirio tu. Mnamo Agosti 2012 kulikuwa na kadirio la asilimia 46.8 za Warusi kuwa Wakristo [12] na asilimia 25 waliamini uwepo wa Mungu lakini bila kufuata dini yoyote. Makadirio mengine yalitaja asilimia 76 za Warusi kuwa Wakristo [13] au asilimia 65 [14].

Upande wa Wakristo, wengi wanakadiriwa kuwa Waorthodoksi (kati ya hao wengi hawashiriki kwenye ibada za mara kwa mara) na wachache ni Wakatoliki na Waprotestanti.[15]

Hekalu la dini zote mjini Kazan, Tatarstan

Uislamu ni dini yenye wafuasi wengi baada ya Kanisa la Kiorthodoksi.[16] Ni dini kuu kati ya watu wengi wa Kaukazi kama vile Wachecheni, Waingushi na Wacherkesi, pia kati ya wasemaji wengi wa Lugha za Kiturki kama vile Watatari na Wabashkiri. Kwa jumla kuna kadirio la kuwepo kwa Waislamu milioni 9.4 ambao ni sawa na asilimia 6.5% ya wananchi wote. Walio wengi ni Wasunni, pamoja na wafuasi wachache wa Shia na Ahmadiya. Sehemu kubwa wanajihesabu kuwa Waislamu bila madhehebu.[17] [12][18]

Katika maeneo matatu kuna wafuasi wa Ubuddha ambayo ni Buryatia, Tuva na Kalmykia.

Dini za jadi hufuatwa bado katika sehemu za Siberia na Mashariki ya Mbali kama vile Yakutia na Chukotka.

Kwa jumla Waslavi mara nyingi ni Wakristo wa Kiorthodoksi, wasemaji wa lugha za Kiturki ni zaidi Waislamu, na wenye lugha za Kimongolia mara nyingi hufuata Ubuddha.[19] Kuhusu watu wasio na dini kuna makadirio kuwa kati ya 16% na 48% ya wananchi wote.[20]

Idadi ya watu wanaojihesabu kuwa Waatheisti ni asilimia 7 na idadi yao imeendelea kupungua. [21]

Từ khóa » Vita Ya Urusi Na Georgia